Zanzibar Police College

MUASISI WA MIRADI MBALIMBALI

DCP ANTONY RUTASHUBURUGUKWA

Unapotembea katika viunga mbali mbali ndani ya chuo cha taaluma ya polisi DPA Jina la RUTTA ni jina maarufu sana, jina la RUTTA limevuka mipaka ya chuo, sasa si ndani  ya chuo tu peke yake hadi maeneo mbalimbali ndani ya Kurasini na maeneo jirani.

DCP Antony Ruttashubukwa alikua ni mkuu wa chuo  wa 21 tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 1961, amekuwa  mkuu wa chuo kwa kipindi cha miaka  miwili, kuanzia tarehe 31.8.2017 hadi   28.11.2019 alipohamishiwa makao makuu ya Jeshi la Polisi kuwa mkuu wa utawala na rasilimali watu.

Ni ngumu kuzungumzia miradi ya chuo pasipo kutaja jina la Rutta, akiwa ni mwalimu kitaaluma (BA)Education kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, mbobevu katika eneo la utawala, ni mtaratibu asiye na maneno mengi lakini mwingi wa vitendo.

Kwa miaka mingi chuo cha Taaluma ya polisi DPA imekua haina miradi ya maana yenye kuweza kuingizia chuo kipato, chuo kimekua kikijiendesha katika mazingira magumu kwa kutegemea pesa ndogo ya uendeshaji kutoka makao makuu, pia ikumbukwe katika utawala wa awamu ya tano chini ya hayati Rais Johhn Pombe Magufuli msisitizo mkubwa uliwekwa katika uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya kuingiza kipato kwa taasisi za serikali.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP Simon Nyankoro Sirro akatoa maelekezo kwa wakuu wa chuo kuwa hatatoa hata shilingi moja za uendeshaji wa chuo, hivyo akae afikirie afanye nini ili kuwa na kipato cha kujiendesha, CO Rutta (DCP) anasema alikua hana namna ya kukwepa maelekezo ya IJP zaidi kuumiza kichwa na kufikiria nini cha kufanya.

Ilikuwa ni vigumu sana kusimamia taaluma wakati huo huo kuhakikisha miradi inaanzishwa na kusimama, akiwa na safu yake ya uongozi kwa wakati huo Mnadhimu mkuu akiwa ACP Kitebo (Marehemu), na mkufunzi mkuu ACP Satta, halikadhalika Insp Rogders ambae alikua mkuu wa miradi kwa wakati huo mambo yalikwenda vizuri sana chini ya usimamizi wao. Walipokea maelekezo ya Mkuu wa chuo hivyo kazi ya kubuni miradi mbalimbali na utekelezaji wake ulianza mara  moja

Katika mahojiano yetu na DCP Rutta, anabainisha kuwa miradi yote ambayo walianzisha ilitokana na fedha kidogo za ndani ya chuo, anasema   “..Tulijibana sana kwani tulidhamiria kuanzisha miradi kwa kile kidogo tulichokuwa nacho na kwa kutumia wadau werevu, na tulifanikiwa kuanza na miradi midogo midogo kama ya bustani, kufuga ngo´mbe wa maziwa, bwawa la samaki, badae miradi ikaendelea kuogezeka tukaanza kupata miradi mikubwa kama Ujenzi wa ukumbi wa sherehe na mikutano RUTTA PARK, Mradi wa jiko na sehemu ya vinywaji, mradi wa ulengaji shabaha nk…..”

Wakuu wa chuo waliofuata waliendelea kusimamia miradi hii, na miradi imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, kwa sasa chuo kina miradi ya Rutta Park (Ukumbi, Rutta Bar and restaurant), Rutta berber shop, Rutta Car wash, Mradi wa udereva, mradi wa ufugaji samaki, mradi wa ng´ombe, duka la chuo, mradi wa bustani, Gym, Uwanja wa mpira, mradi wa ulengaji shabaha.